Thursday, December 15, 2022

DHANA YA MUZIKI WA HIP-HOP NA UHUNI

DHANA YA MUZIKI WA HIP-HOP NA UHUNI

-George Kyomushula

 

Muziki huu wa aina ya HIPHOP uliobeba dhana ya muziki wa wahuni, tangia kuanzishwa kwake miaka ya 1980 huko Marekani. Umesababisha uzorotaji mkubwa wa uwasilishaji kwake kwa jamii katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni duniani, hususani hapa Tanzania. Uzorotaji, uliosababishwa na makisio mabaya kwa jamii , hususani ktk mlengo wa kimaadili hasa ya kibiashara baina ya wadau na wasanii husika wenye falsafa zao na muziki wao

Kisanaa, kila msanii lazima awe na falsafa yake katika kuwasilisha sanaa yake. Falsafa husika ndiyo hutengeneza utambulisho wa msanii husika, siyo tu kwenye muziki hata katika sanaa nyinginezo mathalani  uchoraji, uandishi, uigizaji nk . Kwa mfano Tanzania tunajivunia mtu kama Edward Said Tingatinga na michoro yake ya Tingatinga , Mrisho Mpoto na falsafa yake ya ujomba katika sanaa yake ya Umanju wa mashairi nk. Au kundi moja maarufu kupata kutokea la muziki wa asili la Tatu Nane na utambulisho wao wa kifalsafa za kimakonde kupitia muziki wa asili. Wote hao kama wasanii , ni mfano wa usanii na falsafa husika. Maana kila msanii mwenye falsafa yake katika sanaa yake, hupata kuwa na utambulisho wake kwa hadhira yake.

Falsafa kuu ya muziki wa hiphop wakati unaanzishwa , ilikuwa ni kusadifu dhima ya ukombozi. Ukombozi wa kiuchumi, siasa , mapenzi , uongozi nk. Kila msanii aliamua kuwa na fasafa yake. Ila dhima kuu ilianza na dhima ya ukombozi, ndiyo maana mwanamuziki nguli wa Bongofleva ( zao la muziki wa hiphop lililoasisi lugha ya Kiswahili ) bwana Joseph Mbilinyi , maarufu kama Too Proud au Sugu ( jina alilojipatia enzi za tamthilia maarufu ya Kikenya ya Tausi , miaka hiyo. Kulikuwa na mtoto wa mitaani aliye mtukutu kupata kutokea. Aliyeitwa Sugu, alisumbua Watoto wenzie wa mitaani ) Too Proud au Sugu akiwa kama msanii wa muziki wa bongo fleva, mwenye usugu wa kifalsafa ya ukombozi katika mashairi & nyimbo zake.

 

 

Falsafa yake ndiye iliweza kutambulisha sanaa yake kwa usahihi wa maudhui yake, nyimbo zake sio tu zilikuwa zina nasibu utambulisho wake, bali dhamira yake. Mfano wa nyimbo kama HAKI aliyoimba na Justin Kalikawe ilinasibu uhalisia wa dhamira na ndoto zake baada ya kuja kuwa mbunge baadae, pia MIKONONI MWA POLISI ni kama ilibashiri matatizo yake baadae, mpaka kuingia matatani na jeshi la polisi akiwa mbunge. Kiusanii, msanii mwenye falsafa yake na akafanikiwa kuifanya kuwa utambulisho wake kisanaa. Huwa anakuwa amefanikiwa sana kusadifu utambulisho wake kisanii kwa jamii.

Nimemtolea mfano bwana Joseph mbilinyi ( SUGU ) japo hapa nyumbani Tanzania tulipata bahati ya kuwa na makundi mengi , na wasanii wengi wa muziki huo waliopata kuwa na falsafa tofauti tofauti, nao pia walipata kadhia ya kuhusishwa na uhuni ktk jamii. Kutegemeana na aina ya mavazi yao, uwasilishaji wa sanaa yao kupitia mashairi yao kwa mtindo wa lugha zao zenye rejesta za msimu , vijiweni nk

 

 

 

 

 

MKINGAMO WA FALSAFA YA MSANII NA MATAKWA YA JAMII

Kazi kuu ya msanii ni kuburudisha, elimisha na kuonya. Kwa bahati mbaya, jamii ya sasa inategemea kitu kimoja tu toka kwa msanii ambacho ni kuburudishwa. Jamii kwa ukubwa na upana wake, imefikia namna ya kupangiwa cha kusikiliza, furahia na kuburudushiwa nacho. Hapa ndipo dhana ya muziki wa hihop na uhuni inapoingia na kuonyesha kufanikiwa kwa walioianzisha dhana hiyo kwa malengo binafsi kwa kuipotosha au kuirubuni jamii husika kuwa na mlengo hasi na aina hiyo ya muziki kwa jamii hiyo.

Washika dau duniani kote walifanikiwa kuaminisha duniani kote kuwa HipHop, hususani hapa Tanzania. dhana hii lishamiri kwa sababu ya upya wa utamaduni huo , bila shaka dhana hiyo ya uhuni ilikuwapo kipindi ambacho wazazi wa wazazi wetu walipon’gamua utamaduni wa muziki kama wa Rock N Roll, Jazz , Rhumba, Salsa , Pop , Funky nk

 

Iweje dhana ya hiphop ni uhuni idumu? Pasi na shaka washikadau waliona kadhia ya muziki huo baada ya muda Fulani utakuwa ni ngumu kuutawala kama watapatiwa nafasi ya kutosha vijana wenye kupenda muziki huo ikiwa falsafa ya mziki wao una dhamira ya ukombozi ndani yake. Pengine waliona mbele , kupatia au pengine walikosea . Hiyo itategemea na uelewa wa kila mtu pasi na nafasi yake ya kufanya marejeo ya kifikra penye mantiki na fakti katika jambo hilo. Uhuni pandikizi wa kuwanyon’gonyesha wanamuziki hao vijana kupitia madawa ya kulevya na vileo vingine , havikuja kwa bahati mbaya kama inavyojulikana wanaharakati wote waliopata kutokea .Walifanyiwa ujasusi waliowahi kufanyiwa waasisi wa dhima ya ukombozi wa jamii yao. Kadhia waliyoipata ni kuundiwa zengwe la kijasusi na muasisi wa FBI Edgar J. Hoover aliyoiita COINTELPRO – Counter Intelligence Program iliyonuiwa kunyon’gonyesha, haribu, gombanisha, gawanyisha , piganisha wanaharakati wote wenye dhima ya kimapinduzi  (civil rights movement ). Pengine maafa yaliyotokea miaka hiyo ya 1960 mpaka 1970 kwa wazee wao yameweza kuikumba jamii ya vijana walioanzisha utamaduni wa muziki wa hiphop, kuhusishwa na uhuni kizazi na kizazi duniani.

 

Usisite kuniandikia maoni yako

kyomushula@gmail.com

0717470007

George Kyomushula